HOTUBA YA
UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA SITA WA KAUKI
JUNI 25 –
26, 2010, MAGUBIKE – IRINGA
Ndugu Mgeni Rasmi,
Ndugu Wageni Waalikwa
Ndugu Wanaukoo na Jamii yote inayounda ukoo wa
Kivenule
Ni furaha na matumaini yangu kuwa, wote mliopo katika
hadhira hii ni wazima wa afya na kuwepo kwenu pia kuonesha jinsi mnavyothamini
shughuli ambayo tutaifanya kwa siku mbili, yaani leo na kesho katika
kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI unafanikiwa.
Ndugu Mgeni Rasmi;
Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ulioanzishwa rasmi Desemba 17-18,
2005 Kijijini Kidamali. Harakati za kuanzishwa kwa KAUKI zilianza mwezi
Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa kufanya mkutano wa kwanza wa
mashauriano. Harakati nyingine na kuunda kamati za maandalizi zilielekezwa
upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa upande wa Kidamali, Mkutano wa kwanza
wa maandalizi ya Mkutano Mkuu ulifanyika mwezi Mei ambapo wajumbe toka Dar es
Salaam walishirikia katika majadiliano, kuchagua viongozi wa kuunda kamati ya
maandalizi kama sehemu ya kuhamasisha.
Ndugu Mgeni Rasmi; Umoja wa Ukoo wa Kivenule
ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule
uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006 katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali,
Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, kulienda sambamba na
uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa
Ukoo wa Kivenule na kuwa Katiba Rasmi; hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa shughuli
za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine,
katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo, kulifanya uchaguzi wa Viongozi wa Kanda,
uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.
Ndugu Mgeni Rasmi; Huu ni Mkutano Mkuu wa Sita wa
KAUKI; na tayari mikutano mingine mitano imekwisha fanyika, mitatu kijijini
Kidamali na mkutano moja kijijini Irole na Nduli. Kwa utaratibu uliokubalika
katika Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI na wa Tatu kuwa itabidi mikutano hii pia
ifanyike sehemu nyingine. Na leo hii ni zamu yenu na ndiyo maana mkutano huu
unafanyika hapa Magubike. Katika Mkutano Mkuu wa Tano wa KAUKI uliofanyika
Nduli, washiriki wa mkutano huo kwa pamoja walikubaliana kuwa Mkutano Mkuu wa
Sita ufanyike Magubike.
Malengo ya KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; Malengo makuu ya KAUKI ni kujaribu
kwa kila hali kwa kutumia ujuzi na maarifa, kuinua uwezo wa kielimu, kiuchumi,
kijamii na kimaisha, kwa wanajamii wanaunda umoja huo, kwa kutumia rasimali
mbalimbali zinazopatika katika nchi ya Tanzania na hususani katika maeneo
wanayoishi; ikiwa ni pamoja kuihamasisha jamii hii kufanya kazi kwa juhudi na
maarifa ili kupunguza umaskini unaowakabili.
KAUKI ipo ili kujitahidi kukidhi shida na mahitaji
ya jamii iliyounda umoja huu na hususani katika maeneo lengwa ya elimu, afya,
uchumi na jamii, kwa kushirikisha mawazo, fikra, ujuzi na maarifa ya kila
mwanaukoo, katika mikutano mikuu na mikutano midogo midogo, ambayo inaandaliwa
na wanaukoo wenyewe. Kwa kukutana pamoja, fikra za kujenga, ujuzi, uzoefu,
kujengewa uwezo na maarifa, huunganishwa pamoja na kisha kupanga mikakati
mbadala ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha.
Ndugu Mgeni Rasmi; malengo mengine ya KAUKI ni:
·
kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda
·
Kuisajiri KAUKI na kuwa na mfuko wa kusaidia ndugu katika elimu, afya
na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa na unaendelea kuchangiwa.
·
kuwa na sanduku lake la posta, tovuti. Kwa sasa ina tovuti inayopatika kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com
·
Kuwa na Akaunti katika Benki – tayari imefungua katika Benki ya NMB,
Iringa Mjini
·
kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti
·
kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika
mikutano yake
·
kubuni na kutekeleza miradi ambayo itawasadia wanajamii. Mradi wa
Alizeti-Irole
·
kuwa na kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya
shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja na miradi mbalimbali. Ipo katika
mchakato.
·
Kuchapisha kitabu toleo la kwanza cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa
kipindi cha mwaka 2009-2010. Kazi inaendelea na taarifa mbalimbali tayari
zimekusanywa.
Mafanikio
Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imefanikiwa kufanya
yafuatayo:
·
kuendelea kufanyika kwa mikutano. Mikutano Mikuu mitano tayari
imefanyika Kidamali mara tatu, Irole na Nduli
·
kupanua wigo wa ushiriki kutoka Irole, Nduli, Itagutwa na Mufindi.
·
ufahamu na uelewa wa watu kuhusu KAUKI na mada zinazofundishwa
·
kufahamiana baina ya wana-KAUKI kumeongezeka mara dufu
·
Kuanzishwa kwa Mfuko wa KAUKI
Changamoto
Ndugu Mgeni Rasmi; Changamoto zinazoikabili KAUKI ni
pamoja na
·
Ushiriki duni wa wanaukoo katika mikutano mikuu
·
Spidi ndogo na moyo wa kuchangia mfuko wa kusaidia wanaukoo
·
Kutokidhi gharama za kuandaa mikutano hii kwa sababu michango inakuwa
ni kidogo
·
Kutofikia malengo ya mipango tunayojiwekea
·
Ndugu wa mijini kuwa na mioyo migumu ya kuunga mkono jitihada hizi
Matarajio katika Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; Kama Ratiba inavyoonesha, hayo
ndiyo yatakayofanyika katika siku mbili za Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI.
Lakini, tunategemea kuwa na Mada kadhaa ikiwemo ya Chimbuko Historia ya Ukoo
ambapo tutaijadili kwa undani zaidi. Lakini pia, masuala mengine mfano elimu,
maendeleo na ushirikiano wa dhati baina ya wanandugu yatapewa kipaumbele.
Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na
kila ndugu/mwanaukoo atakuwa na kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake.
Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa
utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau
wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.
Tutakuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli
mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi.
Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu wa Tatu, Nne na wa Tano wa KAUKI, maeneo
yatakayotolewa uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo
mbalimbali. Kwa kupeana elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na
hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo
ni mbadala kwetu. Pia taarifa hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine
kupata mwanga wa shughuli mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha
maisha.
Matarajio ya mbeleni
Ndugu Mgeni Rasmi; Mipango ya KAUKI kwa mwaka
uliopita 2009 na 2010
·
Kuwa na ofisi yenye vifaa kama vile compyuta, printa na fenicha
·
Kuchapisha kitabu cha historia ya wahehe ambapo ndani yake pia kutakuwa
na taarifa za KAUKI
·
Kuongeza wigo wa ushiriki katika mikutano; na
·
Kuhamasisha wana-KAUKI kuchangia mfuko
Hitimisho
Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imeendelea kujikita katika
kuongeza uangavu na weledi kwa wanaukoo kutokana na kutambua changamoto
mbalimbali zinazojitokeza katika dunia hii ya utandawazi. Mazingira na hali
halisi iliyopo ambayo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au kuathiriwa
nayo ni vigezo tosha. Propaganda na kejeli kama kauli mbiu kutoka kwa watu
mbalimbali duniani hususani kwa wanasiasa wetu yameendelea kuwaathiri
wana-KAUKI na watanzania kwa ujumla. Tatizo la ufisadi wa raslimali za
watanzania mkiwemo ninyi, rushwa katika huduma za jamii mfano kukosa dawa
hospitalini, maji safi ya kunywa, elimu duni na ukosefu wa ajira, vyote vinatuathiri
sisi. KAUKI inaamini kuwa mwana-KAUKI mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya
kuamua hatma na mustakali wa maisha yake ya sasa na baadaye. KAUKI haitarajii
maisha bora kwa kila mwana-KAUKI au mtanzania mwingine yataletwa na wanasiana
au watu baki waliopo nje ya nchi yetu. Jukumu la maendeleo ni letu sisi
wenyewe. Ndio maana tunahimiza watu kujitoa kwa hali na mali kuuchangia mfuko
wetu ili uweze kuisaidia jamii yetu katika nyanja zote za kiuchumi, elimu, afya
na maendeleo.
Ndugu Mgeni Rasmi, baada ya kusema hao machache, kwa
niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu ya Magubike, Nakuomba Ufungue
Rasmi Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI).
Karibu Sana
Mwenyekiti
Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu
No comments:
Post a Comment