Asili ya Wahehe wenye mchanganyiko wa Uhabeshi na simulizi zao kwa kuchunguza
mchanganyiko wao na kizazi cha Kingazija.
Makundi mengine ya Wanitole ‘Wahabeshi’ ya Wahehe, ni pamoja na Vahafiwa
walioishi sehemu za Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalangombe,
Ibanangosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe, Welu na Isanzala. Mtawala wao alikuwa Mwalyelu aliyetawala Welu hadi Pawaga ‘Mavaga’ na Mwamwano
Mwansige aliyetawala Wutinde.
Majina ya watu wa kundi hili yalitokana hasa na kufa kwao kwa wingi kwa njaa na maafa,
hawa ni kina Mwamugovano, Mwamaliga, Mwamukemangwa na Mwamuhesa.
Husalimiana ‘kamwene
hafiwa’ au ‘kamwene muponela’ ila kina Mwachaula husalimiana ‘kamwene
lugome’. Vanyatengeta ni kundi
lililoshi maeneo ya Uzungwa, Kitelevasi na Lundamatwe.
Hawa walikuwa ni mafundi wa kufua chuma, walioishi kwenye milima yenye asili ya milipuko ili
kutafuta mchanga wenye chuma, baadhi yao ni kina Mwachusi na Mwamuvange.
Salamu yao ni ‘kamwene tegeta’ ila kina Kalinga husalimiana ‘kamwene higo’, wao hawali mbawala.
Vanyakilwa ni watu walitokea Kilwa na
kuishi maeneo ya Mufindi,
hawa ni kina Mwalwagi na Mwakihwele,
salamu yao ni ‘kamwene kilwa’. Vasavila waliishi juu ya milima ya Welu sehemu za Makungu, Magubike
na Matogalu, hawa ni kina Mwamfilinge na Mwakasike.
Vadongwe ni kundi lililoishi
pembezoni mwa vilima katika maeneo ya Uhambingeto,
Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Wao ni mchanganyiko wa Wanitole na Wasungwa na
salamu yao ni ‘kamwene huvi’. Baadhi yao ni kina Mwamuyovela, Mwamaluvanga na Mwamukakilwa.
Makundi haya ya Wahehe
yanadhihirisha kuwa, wao ni mchanganyiko wa vizazi vya watu wa jamii tofauti
tofauti. Hebu tuone mathalan, jinsi damu
ya Kingazija ilivyoingia kwa Wahehe
na kuleta utawala wa Muyinga, kizazi
cha kina Mkwavinyika (Mkwawa).
Wenyeji wa asili wa Iringa kabla ya Mwamuyinga
kuingia na kuanza kutawala, ni Wasungwa,
ukiwaacha Wanitole kwa mujibu wa
historia halisi iliyovurugwa na tawala za vikundi vya hao Wanitole.
Wasungwa huishi katika safu ya milima ya Usungwa iliyopo mashariki ya mji wa Iringa. Mwamuyinga ambaye pia ana majina ya Mbunsungulu, Mwakilyemikongi,
Muhumba, Mdagaluhando na Lwimato,
yaliyotokana na taabu alizozipata kutoka Ukaguru
hadi Mahenge, lakini jina lake
halisi ni Hasani Yusufu, mjukuu wa Hasani
Hasani, mtu aliyetokea Ungazija kupitia Ushelisheli hadi pwani ya Afrika ya Mashariki,
akitafuta vipusa, pembe za ndovu na kufanya biashara ya
utumwa kama ilivyokuwa kawaida ya Waarabu
wengi wakati huo.
Alifika Kilwa
Kisiwani na kushinda vita alivyopigana na kulowea huko kwa kuoa mwanamke wa
Kiafrika aliyemzalia mtoto aitwaye Yusufu Hasani, aliyerithi usultani wake
hapo baadaye na kumuoa mwanamke wa
Kiafrika pia aliyekuwa binti Mulimba
na kuzaa nae watoto wawili wa kiume, Hasani au ‘Mbunsungulu’ na Ahmad.
Yusuf Hasani aliondolewa mamlakani na kuuawa na
Wareno waliokuwa wanapiga vita utumwa. Hasani ‘Mbunsungulu’ na nduguye Ahmad walikimbilia Mafia
walikopendwa sana na wenyeji wa huko na walianza kutawala huko, ambako Mbunsungulu alioa.
Wakati mkewe akisubiri kujifungua, taarifa za Wareno
kutaka kuwafuata na kuwaangamiza baada ya kugundua kuwa wako huko, ziliwafikia
kupitia kwa mjomba wao, Malik Sud,
aliyenusurika kwenye mapambano Kilwa
Kisiwani. Kwa hiyo, iliwalazimu Mbunsungulu,
Ahmad na mjomba wao kukimbilia Ukaguru karibu na Kilosa.
Kabla ya kuondoka, Mbunsungulu alimuusia mkewe
kuwa mtoto akizaliwa aitwe Wakinakuonewa.
Mbunsungulu alioa tena huko
alikokimbilia na mkewe alimzalia watoto watatu, Ngulusavangi,
Mufwimi na Ngwila.
Mama huyo alihama na kukimbia na watoto wake kutoka Ukaguru kuelekea Upogoroni, maeneo ya Ulanga
huko Mahenge, baada ya Mbunsungulu, Ahmad na mjomba wao, kuvamiwa
na Waarabu na kuuawa.
Vijana hao watatu wakaondokea kuwa wawindaji hodari
sana huko walikokimbilia na walikuwa hawanywi maji ya mito, kila jioni
walichimba visima. Ugomvi uliowatenganisha ulitokana na jambo hilo pamoja na
kitendo cha Ngwila kutangulia kuoa
kabla ya kaka zake Ngulusavangi na Mufwimi bila ya idhini yao.
Kuna habari nyingi za vijana hawa wote watatu,
lakini tutajihusisha zaidi na Mufwimi
ambaye uzao wake ndio ulimleta Muyinga.
Mufwimi aliendelea na uwindaji akiwa na wafuasi wake Mwilapwa,
Mafumiko na Mabiki pamoja na mbwa wawili;
Ludoviko na Muhepapakwima.
Alisafiri hadi Dabaga
katika maeneo ya Ng’uluhe akifikia
kwanza Ikombagulu alikowaacha
wafuasi wake kwa muda na kuendelea mbele kuwinda katika eneo lililotawaliwa na Mwamududa. Huyu bwana alikuwa na uwezo wa kuua nyati hata kumi kwa
siku, aliichoma nyama porini na kuipaka chumvi na kumtumia mtawala Mwamududa
na kwa kuwa watu wa huko hawakuwa wanaijua chumvi bado, Mwamududa alipoipata nyama
hiyo iliyotiwa chumvi aliiona tamu sana.
Chumvi ilimfanya Mufwimi apendwe na kupewa ruhusa ya
kuwinda atakavyo na
alipokaribishwa, aliomba mahala pa kulala akapewa nafasi nyumbani kwa mtawala Mwamududa. Huko alianza kufanya mapenzi
ya siri na binti wa Mwamududa
aliyekataa kuolewa na wanaume wengi waliojitokeza kumposa, hatimaye alimpa
mimba. Alipoambiwa juu ya mimba hiyo na yule binti, aliagiza mtoto akizaliwa
salama akiwa wa kiume aitwe Mwamuyinga
na akiwa wa kike aitwe Semuyinga.
Mwiko wake asile funo, mnyama mdogo wa porini jamii ya mbuzi
na nyakihuko, mnyama afananaye na panya. Pia asiokote kuni za mti uitwao munyatomaa na kukokea moto. Mufwimi alitoroka usiku kwa kuogopa kuuawa na Mwamududa ambaye kumbe alipopata taarifa za ujauzito wa binti yake,
alifurahi sana kwa kujua kuwa sasa angeolewa kirahisi. Mufwimi hakuwarudia tena wale wafuasi wake bali aliendelea kuwinda
hadi huko Itamba, Usungwa alikouawa na nyati.
Wafuasi wake walipomtafuta, walipata taarifa za
kuuawa kwake huko Itamba, lakini pia
walipewa taarifa ambazo Mufwimi
aliwasimulia wakazi wa huko juu ya binti wa Mwamududa aliyemwacha na ujauzito wake.
Waliamua kwenda huko kwa kujifichaficha, lakini
walipodhihirika, walikaribishwa vizuri na kupewa makazi na mtawala Mwamududa aliyefurahi kupata mjukuu.
Huyu Mwamuyinga mtoto wa Mufwimi, chotara wa Kimanga aliyekuwa jasiri tangu ujanani, alimrithi babu yake na kuanza kutawala sehemu hiyo ya Ng’uluhe akiwa ‘Mutwa’ wa kwanza wa kabila lililotoka nje ya Tanganyika.
Ni kutokea kwa huyu Muyinga wa kwanza ndipo ulifuatia mfululizo wa vizazi kupitia kwa
watoto waliozaliwa, ambapo Maliga
alimzaa Mudegela aliyemzaa Kilonge aliyemzaa Ngawona Lupembe
aliyeuawa na mdogo wake Munyigumba,
ambaye alianza kuitanua himaya ya Uhehe baada ya kushika utawala mnamo
mwaka 1870.
Huyu aliwashinda kivita wababe wa Kinitole na kuyaunganisha makabila ya Iringa, watu
waliokuja kuitwa Wahehe na wakoloni
hapo baadaye kutokana na mlio wao wa kivita wanapotupa mikuki kwa kusema he he
he! wakiashiria hatari.
Kutoka Mutwa
huyu ndipo alifuatia kutawala Mukwavinyika,
mtoto wa pili wa Munyigumba, ambaye
jina lake mtawala huyu liliwashinda wakoloni kulitamka na hivyo kufupisha kwa
kutamka Mkwawa.
Mkwavinyika alianza kutawala akiwa na miaka 19 na aliyapiga vita makabila yote
yaliyozunguka himaya yake na kuwashinda watu kama kina Chabuluma, Mtwa wa Wangoni
na Merere, shemeji wa Mtwa wa Wasangu. Mukwavinyika
alipigana pia na wakoloni wa Kijerumani.
Msomaji, simulizi hizi za Wahehe ni ndefu sana na
zenye mambo mengi mno, ikiwemo kujipa majina ya kujitapa kulikofanywa kwa
idhini ya Mutwa baada ya kutenda
matendo makuu, ushujaa wa kutupa mikuki, uwezo wa mbio za kufukuza maadui, dawa
za ushindi wa vita nakadhalika. Kwa sasa hapa panatosha kumalizia simulizi hizi
za Wahehe.
No comments:
Post a Comment