MKUTANO MKUU WA SITA WA
UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)
Kuhusu KAUKI
KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa
rasmi, katika Mkutano Mkuu wa Kwanza Ukoo wa Kivenule; uliofanyika kwa siku
mbili, Kijijini Kidamali, tarehe 17 -18, mwezi Desemba, 2005. Harakati za
kuanzishwa kwa KAUKI zilianza mwezi Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa
kufanya mkutano mkuu wa kwanza wa mashauriano. Mikutano 10 ya mashauriano ilifanyika
kutoka mwezi Februari hadi Novemba, 2005.
Dira ya KAUKI
Kuwa
na jamii elewa, angavu na inayowajibika kwa kujitegemea.
Maono ya KAUKI
Kujengeana uwezo kwa kutumia raslimali, stadi,
ujuzi, maarifa na weledi, kupitia mafunzo, kongamano, mijadala na mikutano ili
kuboresha maisha.
Malengo ya KAUKI
Lengo Kuu
Kuinua na kuboresha maisha ya wanaukoo wa Kivenule,
kielimu, kiuchumi na kimaisha kwa kutumia ujuzi, maarifa na raslimali
zinazotunguka;
Malengo mengine mahsusi
1.
Kuujua na kuuelewa kwa kina Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule;
2.
Kuzikusanya, kuratibu na kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali za Ukoo wa
Kivenule.
3.
Wanaukoo kufahamiana na kutambuana;
4.
Kufanya senza ya ndugu/wanaukoo wanaounda Ukoo wa Kivenule kila
inapobidi kufanya hivyo na Senza hiyo itajumuisha watu waliohai na wafu;
5.
Kuanzisha Mfuko wa Ukoo wa Kivenule utakaosaidia kuinua kiwango cha
Elimu na pia kusomesha wanaukoo wasio na uwezo wa kumudu kulipa ada za shule au
vyuo;
6.
Kuboresha Elimu ndani ya Ukoo wa Kivenule ili ndugu/wanaukoo wawe na
uelewa wa hali juu na kumudu mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika Dunia
ya Utandawazi;
7.
Kusuluhisha na kutatua matatizo yanayojitokeza katika Ukoo wa Kivenule
kwa kupitia vikao vinavyokubalika;
8.
Kuelimisha Wanaukoo/ndugu kuhusiana na madhara ya ugonjwa wa UKIMWI,
matumizi ya Madawa ya Kulevya na Ulevi wa kupindukia;
9.
Kuinua viwango vya maisha vya wanaukoo wa Kivenule na kuishi maisha
mbadala yenye milo kamili, furaha na nyumba bora na nadhifu;
10. Kuongeza na kuimarisha
mahusiano mazuri ndani na nje ya ukoo kwa kushirikiana katika matatizo mfano
raha, ugonjwa, misiba pamoja na majanga makubwa;
11. Kuwa na nguvu ya
kurekebisha tabia zisizostahili kwa wanaukoo/ndugu ndani ya Ukoo na kutafuta
suluhu ya migogoro/migongano baina ya mtu au jamii inayotuzunguka;
12. Wanaukoo kuutambua na
kuuelewa mtawanyiko/mgawanyiko wa Ukoo wa Kivenule;
13. Wanaukoo/ndugu kushirikiana
katika shughuli za uzalishaji mali pamoja na utendaji kazi wa kila siku;
14. Kushirikiana na umoja au
vikundi vingine vilivyoungana ili kuuletea Ukoo wa Kivenule maendeleo endelevu;
15. Kuanzisha Mfuko wa
kukopeshana (SACOSS);
16. Kupunguza au kuondoa kabisa
tabia ya uvivu na uzembe ndani ya Ukoo wa Kivenule; na
Kuanzishwa kwa KAUKI
Harakati za
kuanzishwa kwa KAUKI zilianza kwa kuratibu mawazo ya wana-ukoo wawili, yaani
Ndugu Faustino Kivenule na Ndugu Christian Kivenule mwezi Desemba 2004. Mawazo
hayo yalifanyiwa kazi kwa kumshirikisha Ndugu Adam Kivenule, ambaye bila
kuchelewa, waliweza kuandaa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mashauriano, jijini Dar
es Salaam. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa River Side, tarehe 6
Februari, 2005 – jijini Dar es Salaam.
Harakati
nyingine za maandalizi zilielekezwa upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa
upande wa Kidamali, Mkutano wa kwanza wa mashauriano kwa ajili ya maandalizi ya
Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulifanyika mwezi Mei
ambapo wajumbe toka Dar es Salaam walisafiri kwenda huko ili kuwasilisha hoja,
kufanya mashauriano na majadiliano, kuchagua viongozi wa kusimamia uratibu na kuunda
kamati ya maandalizi.
Maeneo mengine
kama Nduli na Ilole hazikuweza kufanya maandalizi ya moja kwa moja japo taarifa
toka Dar es Salaam ziliweza kufikishwa na baadhi ya wanaukoo wanaishi huko. Mjumbe
mmoja tu ndugu Augustino Kivenule, toka Mgongo ndiye aliyeweza kumudu kushiriki
katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule.
Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI
Huu ni Mkutano
Mkuu wa Sita wa KAUKI; na tayari mikutano mingine mitano imekwisha fanyika, mitatu
kijijini Kidamali na mkutano moja kijijini Irole na Nduli. Kwa utaratibu
uliokubalika katika Mkutano Mkuu wa Pili na wa Tatu wa KAUKI, kuwa itabidi
mikutano hii pia ifanyike sehemu nyingine. Na leo hii ni zamu yenu na ndiyo
maana mkutano huu wa sita unafanyika hapa Magubike. Katika Mkutano Mkuu wa Tano
wa KAUKI uliofanyika Nduli, washiriki wa mkutano huo kwa pamoja walikubaliana kuwa
Mkutano Mkuu wa Sita ufanyike Magubike, leo tarehe 26 na 27 ya Mwezi Juni mwaka
2010.
Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI - Magubike
Ili
kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa Sita unafanyika na kufanikiwa, kila Kanda ililazimika
kufanya maandalizi kwa utaratibu wake. Kwa hiyo kulikuwa na kanda za Kidamali,
Magubike, Irole, Nduli na Dar es Salaam ambazo mara nyingi Uongozi umekuwa
ukipokea taarifa zake. Kila kanda inaelewa majukumu yake ambayo ni pamoja na
kukusanya michango, kuhamasisha ushiriki wa
wanandugu katika Mkutano wa Sita wa KAUKI huko Magubike na pia utoaji wa
michango.
Maandalizi ya
Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI ilibidi yaanze mapema tu mara baada ya kufanyika
kwa Mkutano Mkuu wa Tano wa KAUKI. Maandalizi ya mkutano huu ni jukumu la kila
mwana-ukoo ambapo atashiriki kwa kutoa mchango, nafaka, mfugo au nguvu zake
katika kuhakikisha kuwa maandalizi ya mkutano yanaenda vizuri.
Shughuli za
KAUKI zinafanyika chini ya mwongozo ambao ni Katiba ya Umoja wa Ukoo wa
Kivenule (KAUKI). Katiba hii ilishaanza kutumika mara tu baada ya Mkutano Mkuu
wa Pili wa KAUKI uliofanyika tarehe 24 na 25 Juni 2006. Nakala kadhaa za KAUKI
tayari zimetolewa, kusambazwa na zinaendelea kutumika.
Kwa mujibu wa Katiba ya KAUKI, kuna viongozi
mbalimbali waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wa Pili. Viongozi hao
wanajulikana kama Viongozi wa Kanda. Kila Kanda ambayo ilikubalika kuwepo,
katika Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI, ina viongozi siyo zaidi ya mmoja.
Viongozi hawa, wanawajibika kwa wanaukoo wanaotoka katika Kanda husika.
Wajibu wa viongozi hawa, ni kushirikiana pamoja na
Viongozi wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule katika kutekeleza masuala mbalimbali ya
maendeleo yanayouhusu ukoo. Pia, ni wajibu wa viongozi hawa, kuwashauri
Viongozi wa KAUKI katika masuala mbambali yanayoukabili ukoo wetu kwa mfano
masuala ya ugonjwa, elimu, uchumi na maendeleo.
Viongozi wa Kanda wana nguvu ya Kikatiba katika
kutimiza wajibu wao na pia wana wajibu wa kuhakikisha kuwa mipango mbalimbali
inayopangwa kupitia Kamati Kuu au Mkutano Mkuu wa KAUKI inatekelezwa.
Viongozi wa ngazi nyingine za juu kama Katibu,
Mwenyekiti, Makamu wa Katibu, Makamu wa Mwenyekiti, Mweka Hazina na Msaidizi
wake, wana wajibu wa kuwahimiza viongozi wa Kanda, kushirikiana baina yao
wenyewe na pia kushirikiana na viongozi wakuu kutekeleza wajibu na majukumu
mbalimbali ambayo yanatukabili.
Kwa mujibu wa KAUKI, viongozi wa Kanda, wana wajibu
kuhudhuria vikao mbalimbali kama inavyoainishwa kwenye Katiba ya KAUKI. Wajibu
huo pia unawagusa viongozi wengine wa KAUKI na wanawajibika ipasavyo kutekeleza
na kutimiza wajibu wao.
MICHANGO YA MFUKO WA KAUKI
Kama ilivyokubaliwa kwenye Mkutano Mkuu wa Pili wa
KAUKI na kama Katiba inavyoeleza, kila mwanaukoo, anawajibika kulipa michango
kama inavyoanishwa kwenye Katiba ya KAUKI . Katiba ya KAUKI inafafanua kwa
mapana kuhusiana na michango hiyo ya kila mwezi. Katiba ya KAUKI, inaeleza wazi
kuhusiana na wajibu wa kila mwanaukoo kuchangia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa
KAUKI (Ibara ya 5:3(ii). Matumizi ya michango hiyo ni kuwasaidia wanaukoo
katika matatizo mbalimbali ya ugonjwa, masomo na pia kiuchumi pindi mfuko huo
utakuwa umetuna kutokana na kila mwanaukoo kuuchangia ipasavyo. Pia michango
hiyo itasaidia gharama mbalimbali mfano kufanya mikutano.
Viongozi wa Kanda, walipewa jukumu la kukusanya
michango hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano Mkuu wa Tatu
wa KAUKI, stakabadhi zikiwa na mhuri wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), zilisambazwa
kwa viongozi husika wa Kanda kwa ajili ya shughuli za ukusanyaji wa michango
hiyo. Kila anayetoa mchango ni lazima apewe stakabadhi ya malipo halali na si
vinginevyo.
Taarifa kuhusiana na suala la michango, viongozi wa kanda
watatoa taarifa zaidi.
Lakini viwango hivi vinavyotajwa kwenye Katiba havimfungi
mwanaukoo kutoa zaidi. Mara nyingi katika utoaji wa michango kwa ajili ya
maandalizi ya Mikutano Mikuu, kadi huandaliwa na kusambazwa kwa wana ndugu
mbalimbali na pia kwa jamaa na marafiki zetu. Jambo hili ni nzuri kwa sababu
linaonyesha heshima kwa yule unayemwomba atoe mchango wako. Kwa sababu hiyo,
kadi maalum huandaliwa na kila mmoja wetu ambaye anahitaji kadi hupewa kwa
kiwango kile kinachotakiwa.
Pia, viongozi wa KAUKI walipendekeza wanaukoo kuwa
wabunifu katika kutoa michango yao, hii ni pamoja na kutoa bidhaa au mazao
ambayo yatajulikana kama mchango. Kama ni nafaka au mifugo, inaweza kutumika
kama chakula moja kwa moja au ikauzwa na zikapatikana fedha ambazo
zitajumuishwa kwenye bajeti inayoandaliwa.
MICHANGO TOKA VYANZO VINGINE
Tubuni miradi ambayo inaweza kutuboreshea mapato ya
KAUKI na pia kila mwana-ukoo ahusike kikamilifu. Pia, hii kazi kwa viongozi wa
mipango ya maendeleo kuwa wabunifu wa shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Tunaweza
kubuni miradi ya maandazi, chapati, mama lishe, kilimo au miradi yoyote
ambayo mnadhani itatusadia kupata fedha kwa ajili ya kuweza kufanikisha mikutano
kama hii.
TAREHE YA MKUTANO MKUU WA SITA WA KAUKI
Tarehe 26 ya Jumamosi na 27 Jumapili Juni 2010,
ilipendekezwa kuwa ndiyo siku ambapo Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI utafanyike
Magubike.
YATAKAYOJIRI KATIKA MKUTANO MKUU WA SITA WA KAUKI
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano, kutakuwa
na shughuli mbalimbali katika siku mbili za mkutano. Pamoja na mambo mengine,
kutakuwepo na uwasilisha wa mada kadhaa na pia taarifa mbalimbali kutoka kwa
wana-KAUKI na viongozi, mfano:
·
Mada: 1.CHIMBUKO NA HISTORIA YA
UKOO WA KIVENULE
2. CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI
KAUKI KUJILETEA MAENDELEO
3. HISTORIA YA WAHEHE
·
TAARIFA YA UTENDAJI WA KAUKI
·
TAARIFA YA SHUGHULI ZA MAENDELEO KATIKA KANDA
·
KUSOMA RIPOTI YA MKUTANO MKUU WA TANO WA KAUKI
·
UZOEFU WA WANAUKOO KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO
·
MAJADILIANO YA HOJA MBALIMBALI AMBAZO ZIMEWASILISHWA NA
WASHIRIKI KATIKA MKUTANO
·
MAHITAJI YA KAUKI NA JINSI YA KUFANIKISHA KUPATIKANA KWA
MAHITAJI HAYO: Huu ni mjadala wa jumla na kila mjumbe wa mkutano anashiriki
moja kwa moja kutoa mawazo yake. Katibu na watendaji wengine wa KAUKI wana
jukumu ya kuyanakili maswali na majibu yote kwa ajili ya kufanyiwa kazi
·
MAJUMUISHO NA TATHMINI YA MKUTANO
·
MIPANGO NA MIKAKATI YA MBELENI
·
KUTANGAZWA KWA TAREHE YA MKUTANO MKUU WA SABA
·
SHUKRANI
·
KUFUNGA MKUTANO
Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na
kila ndugu/mwanaukoo atakuwa na kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake.
Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa
utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau
wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.
Tutakuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli
mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi.
Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa KAUKI, maeneo yatakayotolewa
uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo mbalimbali. Kwa kupeana elimu
ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri
na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo ni mbadala kwetu. Pia taarifa
hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine kupata mwanga wa shughuli
mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha maisha.
Pia huu ni mwaka wa uchaguzi. Tunategemea kuwa
wana-ukoo wataitumia fursa hii ipasavyo kuwachangua viongozi wanaoona wanafaa
kuiongoza jumuiya yetu.
UCHAGUZI MKUU WA VIONGOZI
WA KAUKI
Taarifa kuhusu uchaguzi wetu tayari ilikwisha tolewa
kwenye tovuti yetu inayoitwa: http://www.tagumtwafoundation.wetpaint.com
/ http://www.tagumtwa.blogoak.com Natumaini ni watu wachache tu wamemudu
kuiangalia na lakini bado kama viongozi tuna wajibu wa kuwatambulisha katika
mkutano huu. Wafuatao ni viongozi wapya waliochaguliwa:
VIONGOZI WAKUU WA KAUKI
1.
Mwenyekiti Donath
Mhapa
2.
Makamu Mwenyekiti
3.
Katibu Mkuu Adam
Kivenule
4.
Katibu Msaidizi Christian Kivenule
5.
Mweka Hazina Justine Kivenule
6.
Mweka Hazina Msaidizi
UCHAGUZI WA WALEZI WA KAUKI
Wafuatao ni Walezi wa KAUKI
§
John Kivenule
§
Augustino Kivenule
VIONGOZI WA KANDA
Kila Kanda itakuwa na wawakilishi wawili
1.
Mwenyekiti
2.
Katibu
3.
Mweka Hazina
Kutakuwa na Viongozi wa
Kamati mbalimbali
A. Mipango na Maendeleo
- Mwenyekiti:
- Katibu:
B. Mahesabu na Fedha
- Mwenyekiti:
- Katibu:
C. Maafa na Matatizo
- Mwenyekiti:
- Katibu:
D. Nidhamu na Maadili
- Mwenyekiti:
- Katibu:
Angalizo: Viongozi wa Kamati ya Mahesabu na
Fedha, watashirikiana na Mweka Hazina katika kuratibu shughuli zote za
ukusanyaji wa michango mbalimbali, wakati wa maafa, wakati wa mkutano mkuu,
mikutano na pia mchango wa kila mwezi.
MIPANGO YA KAUKI
KAUKI inajikita kujiimarisha katika ngazi
zote za kiutendaji, kiuendeshaji na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kielimu,
kisiasa, kimaendeleo, na kimapinduzi. Baadhi ya mikakati KAUKI ni pamoja na:
1.
KAUKI kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za
Kanda ambapo wanaukoo wanadhani ni muhimu kuwa na ofisi. Jambo hili lilishaanza kufanyiwa kazi na pia eneo ambalo
inabidi ofisi iwepo lilishapatikana katika majadilian ya awali ya mwaka 2008.
Viongozi toka eneo ambalo ofisi inabidi ifunguliwe watatuhabarisha zaidi wapi
wamefikia.
2.
Suala na pili ni kupata usajili ili tuwe na fursa ya kufanya shughuli
kubwa zaidi. Bado suala hili lipo katika mchakato, na
taratibu nyingine zote za namna ya kupata usajili zilikwisha fuatiliwa. Ni
matumaini yetu uongozi mpya uliochaguliwa, unalifanyia kazi kazi jukumu hili
muhimu.
3.
KAUKI kuwa na sanduku lake la posta. Bado jambo
hili halijatekelezwa na natumaini hatua za makusudi inabidi zichukuliwe. Hakuna
masharti makubwa zaidi ya kulipa fedha tu. Ni changamoto kwa viongozi wa KAUKI
na nadhani hatuna haja ya kusubiri zaidi ya kuchukua hatua zinazostahili
kulikamilisha hili.
4.
Kuwa na Akaunti katika Benki yeyote. Ufunguzi
wa Akaunti ulikwisha fanyika kabla ya Mkutano Mkuu wa Nne wa KAUKI uliofanyika
Irole. Hima wanaukoo tutoe michango yetu na pia tusaidie kuitunisha akaunti
yetu. Wangapi wanalipa mia tano za kila mwezi? Mnapata stakabadhi? Wangapi
bado hawajalipa? Kwa nini? Hizi ndizo changamoto kwetu. Bila
kujitoa hatuwezi kufanikiwa. Msitegemea watu wachache tu ndio wanaoweza
kubadili maisha ya wanaukoo wote. Inabidi tuunganishe nguvu zetu wote. Wahenga
walisema, ‘Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’.
5.
KAUKI kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti. Bado kutekelezwa kutokana na uhaba wa fedha na pia bado
wanaukoo hawajaonesha mwito wa kutoa michango ya kila mwezi. Hivyo tunawahimiza
kutoa michango hiyo ili baadhi ya mipango na malengo ya KAUKI yakamilike.
Tutafanya harambee ili tuweze kununua vifaa hivyo, mfano Kompyuta na printa
yake. Wangapi mpo tayari kuchangia?
6.
KAUKI kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Tumeanza na sehemu ndogo na mojawapo ni wakati wa mikutano
hii. Lakini bado tunadhani inabidi tutafute fursa nyingine. Kama tungekamilisha
suala la ofisi, natumaini fursa nyingi za kupata masomo kwa wana-ukoo
zingetafutwa kwa hali na mali.
7.
KAUKI kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ambayo itawasadia
wanajamii. Sijapata taarifa rasmi labda viongozi wa
Irole wanaweza kutupa taarifa. Mwenyekiti wa kipindi kilichopita Bwana Nyakunga
aliahidi kuwa wangeanzisha mradi wa alizeti, Sijui walifikia wapi? Tupatieni
taarifa. Tuanzishe mashamba ya KAUKI na kila kanda iwe na shamba lake. Mazao
yatakayopatikana yatatumika kama sehemu ya chakula wakati wa mikutano hii. Na
pia iliyobaki itauzwa na fedha kuwekwa katika mfuko wa KAUKI.
8.
KAUKI kuwa na kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na Kiujuzi ambacho
kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja na miradi mbalimbali. Tunasubiri kukamilika kwa ofisi na kazi itaanza mara moja.
Binafsi nipo tayari kujitolea kuhakikisha tunafanikiwa katika suala hili.
9.
KAUKI kujitangaza kwa asasi nyingine za ndani ya nchi na nje kwa
kutumia teknolojia ya kisasa yaani kuwa na tovuti. Tumeanzisha
tovuti (blog) na natumaini bado
haijafikiwa na wengi. Mpango mzuri ni sisi wenyewe kulisajili jina la KAUKI
(Domain Registration) kwa wamiliki wa mitandao na kuiweka hewani tovuti yetu
kwa watoa huduma za mawasiliano ya tovuti na mitandao.
10. Kuchapisha kitabu toleo la
kwanza cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2008 – 2009. Kamati iliyoundwa imeshindwa kukutana na kuikamilisha kazi
hiyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za:
- Kukosa pesa
- Mtawanyiko wa wajumbe
- Shughuli yenyewe inahitaji pesa kwa mfano kazi ya uhariri na uchapishaji
Kutokana shughuli kuwa ngumu
na kushindwa kufanyika kama ilivyopangwa, inabidi kamati iwasilishe taarifa na
mapendekezo kwa wajumbe kuhusu hatua ambazo imechukua na nini imekifanya; na
pia nini kifanyike, kwa kurejea hadidu zake na pia majukumu yaliyopaswa
kufanyika kabla ya mkutano huu wa tano.
MAPUNGUFU YA KAUKI NA
WATENDAJI WAKE
Uongozi wa KAUKI bado umeonyesha mapungufu na hii
pia inaathiri mfumo mzima wa utendaji kazi zake. Baadhi ya mapungufu hayo ni
pamoja na kushindwa kubisa kutekeleza baadhi ya mikakati ambayo ilikuwa ni
sehemu ya makubaliano na pia mipango ya mbeleni ya maendeleo ya KAUKI. Kwa
mfano baadhi ya majukumu ambayo bado hayajatekelezwa ni pamoja na:-
1.
Kutokuwa na Kalenda ya Shughuli za Mwaka;
2.
Kushindwa kufanya vikao vya Kamati Kuu;
3.
Ushirikiano finyu baina ya viongozi wa ngazi mbalimbali wa KAUKI
kutokuwepo kwa mpango-kazi, tathmini ya utendaji kazi na utekelezaji wa mipango
ya maendeleo;
4.
Viongozi wengi wa KAUKI kushindwa kutekeleza wajibu wao;
5.
Makusanyo hafifu ya michango; Wangapi wamelipa mpaka muda huu?
6.
Viongozi kutokuwa mfano mzuri katika kutoa michango. Tunaamini kiongozi
lazima awe ni mfano wa kuigwa; Je viongozi wote mnatoa michango ya kila mwezi. Wangapi wamelipa
mpaka muda huu?
7.
Wanaukoo kuonesha mwitikio duni katika ushiriki wa Mikutano Mikuu.
Mfano wa Wanaukoo kutoka Dar es Salaam; na
8.
KAUKI kutokuwa na ofisi. Ni mwaka wa pili sasa jambo hili ilibidi liwe
limekamilika lakini mpaka sasa bado ofisi haijaanza kufanya kazi. Hii ni
changamoto kwa viongozi wetu.
VIONGOZI WAKUU WA KAUKI
1.
Mwenyekiti Donath P. Mhapa
2.
Makamu Mwenyekiti
3.
Katibu Mkuu Adam A. Kivenule
4.
Makamu Katibu
5.
Mhasibu Mkuu Justin D. Kivenule
Walezi
1.
Stephan Mhapa
2.
John Kivenule
3.
Augustino Kivenule
HITIMISHO
KAUKI imeendelea kujikita katika kuongeza
uangavu na weledi kwa wanaukoo kutokana na kutambua changamoto mbalimbali
zinazojitokeza katika dunia hii ya utandawazi. Mazingira na hali halisi iliyopo
ambayo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au kuathiriwa nayo ni vigezo
tosha. Propaganda na kejeli kama kauli mbiu kutoka kwa watu mbalimbali duniani
hususiani kwa wanasiasa wetu yameendelea kuwaathiri wana-KAUKI na watanzania
kwa ujumla. Tatizo la ufisadi wa raslimali za watanzania mkiwemo ninyi, rushwa
katika huduma za jamii mfano kukosa dawa hospitalini, maji safi ya kunywa,
elimu duni na ukosefu wa ajira, vyote vinamwathiri sisi. KAUKI inaamini kuwa
mwana-KAUKI mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kuamua hatma na mustakali
wa maisha yake ya sasa na baadaye. KAUKI haitarajii maisha bora kwa kila
mwana-KAUKI au mtanzania mwingine yataletwa na wanasiana au watu baki waliopo
nje ya nchi yetu. Jukumu la maendeleo ni letu sisi wenyewe. Ndio maana
tunahimiza watu kujitoa kwa hali na mali kuuchangia mfuko wetu ili uweze
kuisaidia jamii yetu katika nyanja zote za kiuchumi, elimu, afya na maendeleo.
Yote yanayofanyika katika mikutano hii ni
sehemu ndogo ya jitihada kubwa zinazofanywa na KAUKI. Ahadi za wanasiasa ni za
mdomoni tu na hatuamini hata siku moja kama wana-KAUKI mtayafurahia maisha bora
kwa kukaa mtu moja moja au kwa kutounganisha nguvu zenu. Wanasiasa wana-agenda
zao ambazo mara nyingi huwa kuangalia maslahi yao na kuyalinda. Mfano wa hivi
karibuni kwa Wabunge wameomba kujiongezea mshahara hadi kufikia milioni kumi na
mbili kutoka milioni saba (7) wanazolipwa sasa. Mishahara hiyo ni kodi za
maskini sisi wana-KAUKI na wenzetu ambao hawapo hapa. Kwa hiyo suala la
kujikwamua kimaendeleo la kila mmoja wetu hapa na si vinginevyo. Hizi ni
mojawapo ya harakati za kujikwamua na lindi la umaskini unaotukabili. Lakini
harakati nyingine unazifanya wewe kama mwana-KAUKI wakati wa kupiga kura yako
kumchagua kiongozi. Msilemae na rushwa. Tumieni vizuri fursa yenu kwa kuchagua
viongozi bora. Pengine hata katika chaguzi wa viongozi wa KAUKI watu wanaweza
kutoa rushwa ili wachaguliwe! Tumieni fursa zinazopatikana kwa kuwahoji wale
wanaotaka nafasi za uongozi, nini kimewatuma kugombea nafasi hizo, na sisi kama
wana-KAUKI tutarajie nini. Jamii yetu ni maskini wa kila kitu, wataisaidiaje?
Siasa za porojo zimepitwa na wakati. Kama
wana-KAUKI inabidi kuhimiza mabadiliko ya kiitikadi na kimaendeleo. Wajibu watu
ni kuwadhihirishia nini tunakusudia kukifanya ili kuboresha maisha yetu. Maisha
bora kwa kila mtanzania kama mnavyoahidiwa katika kampeni za uchaguzi ni ndoto
tu.
Kwa mfano huu ni mwaka wa tano toka
uchaguzi mkuu ufanyike na wananchi mliahidiwa maisha bora kwa kila mtanzania.
Je haya maisha mnayoishi kweli ni maisha bora ukilinganisha na maisha mliyokuwa
mnaishi siku za nyuma. Mfumuko wa bei, kupanda kwa bei za mafuta kila wakati,
njaa, ufisadi, dhuluma na kejeli na hata vifo kwa wapigania haki za wanyonge.
Hii ni hali ya kukatisha tamaa na sisi wana-KAUKI tuna kila wajibu na
kukabiliana na hali hii.
Tukikaa pembeni na kuacha yatokee basi
nasi tutaangamia kwani kinachofanyika kinatuathiri sisi. Ufisadi na wizi wa
mali ya umma unatuathiri sisi. Kwa mfano kukosekana kwa huduma za msingi mfano
huduma za afya, shule bora, maji na bei kubwa ya umeme ni matokeo ya dhuluma
hizi. Hivyo kama wana-KAUKI bado tuna jukumu kubwa la kukabiliana na kila aina
ya uozo, na adui wa maisha na maendeleo yetu.
Mbadala ya maendeleo ya nchi ya Tanzania
unakutegemea wewe mwana-KAUKI, dhima, uamuke toka sasa na uelekeze nguvu zako
katika kuiboresha KAUKI ili jamii yetu ipate maendeleo.
Mwisho
Imetolewa na:
___________________________
___________________________
Donath Mhapa Adam
A. Kivenule
No comments:
Post a Comment