MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI

MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI
Tangazo la Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

KAUKI-Kidamali, Iringa

KAUKI-Kidamali, Iringa
Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Tuesday, March 26, 2013

MAPENDEKEZO YA NEMBO YA UMOJA WA UKOO WA KIVENULE-KAUKI

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kuhusu Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule, inaonesha kuwa Babu TAGUMTWA BALAMA (KIVENULE) ndiye aliyewazaa Babu TAVIMYENDA KIVENULE na Babu KALASI KIVENULE. Ikumbukwe kuwa, jina halisi la ukoo wa Kivenule ni BALAMA. Kama ilivyokwisha julikana katika mada iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Kwanza na wa Pili wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ambapo ilielezwa kuwa, neno KIVENULE linamaanisha sifa ya kuwa jasiri Vitani na hasa katika kutumia silaha za Mishale na Mikuki yaani kwa Lugha Asilia ya Kihehe “KUMIGOHA”.  Yaani kwa maana nyingine LIGALU yenye maana ya Kwihoma ImigohaKuhoma Watavangu au Kuvenula Avatawangu. LIGALU maana yake Vita. Kuhoma maana yake Kuchoma na Migoha maana yake Mikuki. Venula maana yake ua, fyeka maadui.

LIGALU ndiyo iliyochangia kuzaliwa kwa jina la Ukoo la KIVENULE. KIVENULE maana yake ni Ushujaa kutokana na Shabaha ya Mikuki.

KUVENULA likiwa na maana halisi ya kuwa na shabaha ya kuwaangamiza maadui kwa kutumia silaha ya Mishale na Mikuki. Babu zetu akina TAGUMTWA BALAMA walilidhihirisha hili katika Vita na Watavangu na hivyo kusababisha kuzawadiwa kwa jina la KIVENULE kama jina la sifa kutokana na ushujaa katika Vita.

Kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa hapo juu kuhusu Chimbuko na Historia ya  Ukoo wa Kivenule, Uongozi wa KAUKI umechukua jukumu mahusui la kubuni na kuchora nembo itakayotumiwa na Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa matumizi mbalimbali. Mapendekezo hayo ya Nembo yana ujumbe ufuatao kama inavyofafanuliwa:
1.     Mkuki na Ngao: Ni ishara ya Silaha za Jadi zilizotumiwa na Babu Tagumtwa huko vitani na kupelekea kuwa shujaa wa Vita na kupewa jina la KIVENULE kama Sifa, Heshima na Zawadi.
2.     Picha ya Watu Wameshikana Mkono: Ni ishara ya Umoja ambao tunaujenga, lakini pia hata Babu zetu walipigania kuurudisha umoja wao ulikuwa umeharibiwa na Vita.
3.     Watu: Ni ishara ya kuwepo kwa jamii ya iliyokombolewa na Tagumtwa ambayo bado ipo mpaka leo na inanufaika na kazi yake, yaani Ukoo wa KIVENULE.
4.     Pembe za Wanyama: Ni ishara ya Raslimali tulizorithi na ambazo ni nguzo ya uchumi wetu na pia pembe nyingine ni zana ambazo zinatumika katika mawasiliano mfano kupiga mbiu…
5.     Ngao ya Kifalme: Ni ishara ya heshima ambayo Ukoo wa Kivenule ilipata kupitia Tagumtwa baada ya kuwa Shujaa katika Vita kwa kuwaangamiza maadui (Avatawangu) kwa mikuki.
6.     Duara katikati ya Nembo lenye Miti ya Kijani, Ardhi Nzuri, Maji na Wanyama: Ni ishara ya urithi ambao tumeupata baada ya harakati mbalimbali za ukombozi ambazo Babu zetu (Tagumtwa) na wengine walizifanya kwa kupigana kiume. Ni Neema ambayo jamii yetu inapaswa kunufaika nayo. Pia ni Ishara ya kutuonesha kuwa ndiko tunakotakiwa kwenda kuishi na kunufaika na Raslimali hizo.
7.     Mwanga wa Jua: Ni ishara ya Nuru na uangavu ambao kila mwana ukoo anapaswa kumulikwa nao. Nuru na uangavu ni taarifa mbalimbali na elimu ambayo kila mwana-KAUKI anapaswa kuipata ili kujikomboa na lindi la Umaskini, Ujinga na Maradhi; na kuweza kuishi maisha mbadala, yaani maisha bora na yenye maendeleo. Nuru inasaidia kuona mbali na hivyo kukupa uangavu kupitia macho na pia taarifa mbalimbali kupitia elimu ya darasani au nje ya darasa na hivyo kuweza kumudu na kuyatawala mazingira yanayotuzunguka.

Hayo ni baadhi ya maelezo mafupi kuhusiana na Mapendekezo ya Nembo ya KAUKI. Kama washiriki wa Mkutano Mnaiunga mkono, mnaombwa kutoa dukuduku na mawazo mbalimbali ambayo yatasaidia kuiboresha na kuwa nzuri zaidi na ya kueleweka.

Napenda kuwasilisha.

Adam Kivenule
Katibu Mkuu

No comments:

Post a Comment