Ndugu
Mgeni Rasmi,
Ndugu
Wageni Waalikwa;
Wanaukoo
na Jamii yote inayounda Ukoo wa Kivenule;
Mabibi na
Mabwana;
Kamwene…,
Munogage…, Makasi…,
Ni furaha
iliyoje kuwa nanyi katika hadhara hii. Ni matumaini yangu kuwa, wote ni wazima
wa afya na kuwepo kwenu pia kuonesha jinsi mnavyothamini shughuli ambayo
tutaifanya kwa siku mbili, yaani leo na kesho katika kuhakikisha kuwa Mkutano
Mkuu wa Saba wa KAUKI unafanikiwa.
Ndugu
Mgeni Rasmi; nianze kutoa historia fupi
ya umoja huu. KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka
2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii
inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia
kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la
umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi. Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ulianzishwa
rasmi mnamo Desemba 17 - 18, 2005 Kijijini Kidamali. Harakati za kuanzishwa kwa
KAUKI zilianza mwezi Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa kufanya mkutano
wa kwanza wa mashauriano. Harakati nyingine na kuunda kamati za maandalizi
zilielekezwa upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa upande wa Kidamali,
Mkutano wa kwanza wa maandalizi ya Mkutano Mkuu ulifanyika mwezi Mei ambapo
wajumbe toka Dar es Salaam walishiriki katika majadiliano, kuchagua viongozi wa
kuunda kamati ya maandalizi na kuhamasisha.
Ndugu
Mgeni Rasmi; Umoja wa Ukoo wa Kivenule ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika
Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006
katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali, Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo
wa Kivenule, kulienda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na
Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule na kuwa Katiba Rasmi;
hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali
ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa
Ukoo, kulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa Kanda, uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na
hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.
Ndugu
Mgeni Rasmi; Huu ni Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI; na tayari mikutano mingine sita
imekwisha fanyika, mitatu kijijini Kidamali na mkutano moja kijijini Irole, Nduli
na Magubike. Kwa utaratibu uliokubalika katika Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI na
wa Tatu kuwa itabidi mikutano hii pia ifanyike sehemu nyingine ambako kuna
jamii inayounda umoja huu. Na leo hii ni zamu yenu na ndiyo maana mkutano huu
unafanyika hapa Igowole, Mufindi. Katika Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI
uliofanyika Magubike, washiriki wa mkutano huo kwa pamoja walikubaliana kuwa
Mkutano Mkuu wa Saba ufanyike Igowole, Mufindi.
Malengo
ya KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; malengo makuu ya KAUKI ni kujaribu kwa
kila hali kwa kutumia ujuzi na maarifa, kuinua uwezo wa kielimu, kiuchumi na kimaendeleo,
kwa wanajamii wanaounda umoja huo, kwa kutumia rasilimali mbalimbali
zinazopatika katika nchi ya Tanzania na hususani katika maeneo wanayoishi;
ikiwa ni pamoja kuihamasisha jamii hii kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili
kupunguza umaskini unaowakabili.
KAUKI imeanzishwa kukidhi shida na mahitaji ya jamii
iliyounda umoja huu na hususani katika maeneo lengwa ya elimu, afya, uchumi na maendeleo,
kwa kushirikisha mawazo, fikra, ujuzi na maarifa ya kila mwanaukoo, katika
mikutano mikuu na mikutano midogo midogo, ambayo inaandaliwa na wanaukoo
wenyewe. Kwa kukutana pamoja, fikra za kujenga, ujuzi, uzoefu, kujengewa uwezo
na maarifa, huunganishwa pamoja na kisha kupanga mikakati mbadala ya kuweza
kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha.
Ndugu Mgeni Rasmi; malengo KAUKI ni mengi na baadhi yake ni:
·
kuwa na ofisi yake Kijijini
Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda
·
Kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa
kusaidia ndugu katika elimu, afya na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa
na unaendelea kuchangiwa.
·
kuwa na sanduku lake la posta,
tovuti. Kwa sasa ina tovuti inayopatika
kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com na inaboreshwa
kupitia www.tagumtwa.blogoak.com
·
Kuwa na Akaunti katika Benki –
tayari imefungua katika Benki ya NMB, Iringa Mjini
·
kuwa na vitendea kazi mfano
Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti
·
kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa
wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake
·
kubuni na kutekeleza miradi ambayo
itawasadia wanajamii. Mpango wa Mradi wa Alizeti-Irole, ambao bado haujaanza
kutekelezwa.
·
kuwa na kitengo cha Utaalam wa
Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja
na miradi mbalimbali. Ipo katika mchakato.
·
Kuchapisha kitabu toleo la kwanza
cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2009-2012. Kazi inaendelea
na taarifa mbalimbali zinaendelea kukusanywa.
Mafanikio
Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imefanikiwa kufanya yafuatayo:
·
kuendelea kufanyika kwa mikutano
mkuu. Mikutano Mikuu sita tayari imefanyika Kidamali mara tatu, Irole, Nduli na
Magubike mara moja moja.
·
kupanua wigo wa ushiriki kutoka
Irole, Nduli, Itagutwa, Mgongo na Mufindi; Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro
na maeneo mengine.
·
Kuongezeka kwa ufahamu na uelewa wa
watu kuhusu KAUKI na mada zinazofundishwa
·
kufahamiana baina ya wana-KAUKI
kumeongezeka mara dufu
·
Kuanzishwa kwa Mfuko wa KAUKI
·
Imeanzisha blogs ambazo zinabeba
taarifa mbalimbali za KAUKI na wana-KAUKI kwa ujumla.
Changamoto
Ndugu Mgeni Rasmi; Changamoto zinazoikabili KAUKI ni pamoja
na
·
Ushiriki duni wa wanaukoo katika
mikutano mikuu
·
Kasi ndogo na moyo wa kuchangia
mfuko wa kusaidia wanaukoo
·
Kutokidhi gharama za kuandaa mikutano
hii kwa sababu michango inakuwa ni kidogo
·
Kutofikia malengo ya mipango
tunayojiwekea
·
Ndugu wa mijini kuwa na mwamko
mdogo wa kuunga mkono jitihada hizi
Matarajio
katika Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; Kama Ratiba inavyoonesha, hayo ndiyo
yatakayofanyika katika siku mbili za Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI. Lakini,
tunategemea kuwa na Mada kadhaa ikiwemo ya Chimbuko Historia ya Ukoo ambapo
tutaijadili kwa undani zaidi. Lakini pia, masuala mengine mfano elimu,
maendeleo na ushirikiano wa dhati baina ya wanandugu yatapewa kipaumbele.
Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na kila
ndugu/mwanaukoo atakuwa na kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake.
Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa
utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau
wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.
Tutakuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli
mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi.
Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu wa Tatu, Nne, Tano na wa Sita wa KAUKI,
maeneo yatakayotolewa uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo
mbalimbali. Kwa kupeana elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na
hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo
ni mbadala kwetu. Pia taarifa hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine
kupata mwanga wa shughuli mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha
maisha.
Matarajio
ya Mbeleni
Ndugu Mgeni Rasmi; Mipango ya KAUKI kwa mwaka uliopita 2010
na 2011
·
Kuendeleza jitihada za kufungua
ofisi Kidamali na kununua vifaa vya ndani ya ofisi kama vile kompyuta, printa
na fenicha
·
Kuchapisha kitabu cha historia ya
wahehe ambapo ndani yake pia kutakuwa na taarifa za KAUKI
·
Kuongeza wigo wa ushiriki katika
mikutano; na
·
Kuhamasisha wana-KAUKI kuchangia
mfuko
Hitimisho
Ndugu
Mgeni Rasmi; KAUKI imeendelea kujikita katika kuongeza uangavu na weledi kwa
wanaukoo kutokana na kutambua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika dunia
hii ya ushindani. Ugumu wa maisha, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, na
changamoto mbalimbali ambazo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au
kuathiriwa nayo. Tatizo la ufisadi wa raslimali za watanzania, rushwa katika
huduma za jamii mfano kukosa dawa hospitalini, maji safi na salama, elimu duni na
ukosefu wa ajira, vyote vinatuathiri sisi. KAUKI inaamini kuwa mwana-KAUKI
mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kuamua hatma na mustakabali wa maisha
yake ya sasa na baadaye. KAUKI haitarajii maisha bora kwa kila mwana-KAUKI au
mtanzania mwingine yataletwa na wanasiasa au watu baki waliopo nje ya nchi
yetu. Jukumu la maendeleo ni letu sisi wenyewe. Ndio maana tunahimiza watu
kujitoa kwa hali na mali kuuchangia mfuko wetu ili uweze kuisaidia jamii yetu
katika nyanja zote za kiuchumi, elimu, afya na maendeleo.
Ndugu
Mgeni Rasmi, baada ya kusema hayo machache, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi
ya Mkutano Mkuu ya Igowole, Mufindi, nakuomba Ufungue Rasmi Mkutano Mkuu wa saba
wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI).
Karibu
Sana
Imetolewa na:
Ndugu Donath Mhapa
Mwenyekiti
Kwa Niaba
ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI
No comments:
Post a Comment