WAHEHE: Ungazija
wa Wanyalukolo
KARIBU msomaji kwa mara nyingine tena
katika safu yetu ya Ndivyo Ilivyo. Wiki iliyopita tuliitambua asili ya Wahehe
wenye mchanganyiko wa Uhabeshi na
niliwaahidi kumalizia simulizi zao kwa kuchunguza mchanganyiko wao na kizazi
cha Kingazija.
Tukiendelea na baadhi ya makundi ya Wanitole ‘Wahabeshi’ ya Wahehe, ambayo sikuyataja wiki iliyopita, ni pamoja na Vahafiwa
walioishi sehemu za Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalangombe,
Ibanangosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe, Welu na Isanzala. Mtawala wao alikuwa Mwalyelu aliyetawala Welu hadi Pawaga ‘Mavaga’ na Mwamwano
Mwansige aliyetawala Wutinde.
Majina ya watu wa kundi hili yalitokana hasa na kufa kwao kwa wingi kwa njaa na maafa,
hawa ni kina Mwamugovano, Mwamaliga, Mwamukemangwa na Mwamuhesa.
Husalimiana ‘kamwene
hafiwa’ au ‘kamwene muponela’ ila kina Mwachaula husalimiana ‘kamwene
lugome’. Vanyatengeta ni kundi lililoshi maeneo ya Uzungwa, Kitelevasi na Lundamatwe.
Hawa walikuwa ni mafundi wa kufua chuma, walioishi kwenye milima
yenye asili ya milipuko ili kutafuta mchanga wenye chuma, baadhi yao ni kina Mwachusi na Mwamuvange.
Salamu yao ni ‘kamwene tegeta’ ila kina Kalinga husalimiana ‘kamwene higo’, wao hawali mbawala.
Vanyakilwa ni watu walitokea Kilwa na kuishi maeneo ya Mufindi, hawa ni kina Mwalwagi na Mwakihwele, salamu yao ni ‘kamwene kilwa’. Vasavila waliishi juu ya milima ya Welu sehemu za Makungu, Magubike na Matogalu, hawa ni kina Mwamfilinge na Mwakasike. Vadongwe ni kundi lililoishi pembezoni mwa
vilima katika maeneo ya Uhambingeto,
Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Wao ni mchanganyiko wa Wanitole na Wasungwa na salamu yao ni ‘kamwene huvi’. Baadhi
yao ni kina Mwamuyovela, Mwamaluvanga na Mwamukakilwa. Makundi haya ya Wahehe
yanadhihirisha kuwa, wao ni mchanganyiko wa vizazi vya watu wa jamii tofauti
tofauti. Hebu tuone mathalan, jinsi damu
ya Kingazija ilivyoingia kwa Wahehe
na kuleta utawala wa Muyinga, kizazi
cha kina Mkwavinyika (Mkwawa).
Wenyeji wa asili wa Iringa kabla ya Mwamuyinga kuingia na kuanza kutawala, ni Wasungwa, ukiwaacha Wanitole
kwa mujibu wa historia halisi iliyovurugwa na tawala za vikundi vya hao Wanitole.
Wasungwa huishi katika safu ya
milima ya Usungwa iliyopo mashariki
ya mji wa Iringa. Mwamuyinga ambaye pia ana majina ya Mbunsungulu, Mwakilyemikongi, Muhumba,
Mdagaluhando na Lwimato, yaliyotokana na taabu alizozipata kutoka Ukaguru hadi Mahenge, lakini jina lake halisi ni Hasani Yusufu,
mjukuu wa Hasani Hasani, mtu aliyetokea Ungazija kupitia Ushelisheli
hadi pwani ya Afrika ya
Mashariki, akitafuta vipusa, pembe za ndovu na kufanya biashara ya
utumwa kama ilivyokuwa kawaida ya Waarabu
wengi wakati huo.
Alifika Kilwa Kisiwani na kushinda vita alivyopigana na kulowea huko kwa
kuoa mwanamke wa Kiafrika
aliyemzalia mtoto aitwaye Yusufu Hasani,
aliyerithi usultani wake hapo baadaye na kumuoa mwanamke wa Kiafrika pia aliyekuwa binti Mulimba na kuzaa nae watoto wawili wa kiume, Hasani au
‘Mbunsungulu’ na Ahmad.
Yusuf Hasani aliondolewa mamlakani na kuuawa na
Wareno waliokuwa wanapiga vita utumwa. Hasani ‘Mbunsungulu’ na nduguye Ahmad walikimbilia Mafia
walikopendwa sana na wenyeji wa huko na walianza kutawala huko, ambako Mbunsungulu alioa.
Wakati mkewe akisubiri kujifungua,
taarifa za Wareno kutaka kuwafuata na kuwaangamiza baada ya kugundua kuwa wako
huko, ziliwafikia kupitia kwa mjomba wao, Malik
Sud, aliyenusurika kwenye mapambano Kilwa
Kisiwani. Kwa hiyo, iliwalazimu Mbunsungulu,
Ahmad na mjomba wao kukimbilia Ukaguru karibu na Kilosa.
Kabla ya kuondoka, Mbunsungulu alimuusia mkewe kuwa mtoto akizaliwa aitwe Wakinakuonewa. Mbunsungulu alioa tena huko alikokimbilia na mkewe alimzalia watoto
watatu, Ngulusavangi, Mufwimi na Ngwila.
Mama huyo alihama na kukimbia na
watoto wake kutoka Ukaguru kuelekea Upogoroni, maeneo ya Ulanga huko Mahenge, baada ya Mbunsungulu,
Ahmad na mjomba wao, kuvamiwa na Waarabu na kuuawa.
Vijana hao watatu wakaondokea kuwa
wawindaji hodari sana huko walikokimbilia na walikuwa hawanywi maji ya mito,
kila jioni walichimba visima. Ugomvi uliowatenganisha ulitokana na jambo hilo
pamoja na kitendo cha Ngwila
kutangulia kuoa kabla ya kaka zake
Ngulusavangi na Mufwimi bila ya
idhini yao.
Kuna habari nyingi za vijana hawa
wote watatu, lakini tutajihusisha zaidi na Mufwimi
ambaye uzao wake ndio ulimleta Muyinga.
Mufwimi aliendelea na uwindaji akiwa na wafuasi wake Mwilapwa, Mafumiko na Mabiki
pamoja na mbwa wawili; Ludoviko na Muhepapakwima.
Alisafiri hadi Dabaga katika maeneo ya Ng’uluhe
akifikia kwanza Ikombagulu
alikowaacha wafuasi wake kwa muda na kuendelea mbele kuwinda katika eneo
lililotawaliwa na Mwamududa. Huyu bwana
alikuwa na uwezo wa kuua
nyati hata kumi kwa siku, aliichoma nyama porini na kuipaka chumvi na kumtumia
mtawala Mwamududa na kwa kuwa watu wa huko hawakuwa wanaijua chumvi
bado, Mwamududa alipoipata nyama hiyo iliyotiwa chumvi aliiona
tamu sana.
Chumvi ilimfanya Mufwimi apendwe na kupewa ruhusa
ya kuwinda
atakavyo na alipokaribishwa, aliomba mahala pa kulala akapewa nafasi nyumbani
kwa mtawala Mwamududa. Huko alianza
kufanya mapenzi ya siri na binti wa Mwamududa
aliyekataa kuolewa na wanaume wengi waliojitokeza kumposa, hatimaye alimpa
mimba. Alipoambiwa juu ya mimba hiyo na yule binti, aliagiza mtoto akizaliwa
salama akiwa wa kiume aitwe Mwamuyinga
na akiwa wa kike aitwe Semuyinga.
Mwiko wake
asile funo,
mnyama mdogo wa porini jamii ya mbuzi na nyakihuko,
mnyama afananaye na panya. Pia
asiokote kuni za mti uitwao munyatomaa
na kukokea moto. Mufwimi alitoroka usiku kwa kuogopa
kuuawa na Mwamududa ambaye kumbe
alipopata taarifa za ujauzito wa binti yake, alifurahi sana kwa kujua kuwa sasa
angeolewa kirahisi. Mufwimi
hakuwarudia tena wale wafuasi wake bali aliendelea kuwinda hadi huko Itamba, Usungwa alikouawa na nyati.
Wafuasi wake walipomtafuta, walipata
taarifa za kuuawa kwake huko Itamba,
lakini pia walipewa taarifa ambazo Mufwimi
aliwasimulia wakazi wa huko juu ya binti wa Mwamududa aliyemwacha na ujauzito wake.
Waliamua kwenda huko kwa
kujifichaficha, lakini walipodhihirika, walikaribishwa vizuri na kupewa makazi
na mtawala Mwamududa aliyefurahi
kupata mjukuu. Huyu Mwamuyinga mtoto
wa Mufwimi, chotara wa Kimanga aliyekuwa jasiri tangu ujanani, alimrithi babu yake na kuanza kutawala sehemu hiyo ya Ng’uluhe akiwa ‘Mutwa’ wa kwanza wa kabila lililotoka nje ya Tanganyika.
Ni kutokea kwa huyu Muyinga wa kwanza ndipo ulifuatia
mfululizo wa vizazi kupitia kwa watoto waliozaliwa, ambapo Maliga alimzaa Mudegela
aliyemzaa Kilonge aliyemzaa Ngawona Lupembe aliyeuawa na mdogo wake Munyigumba, ambaye alianza kuitanua himaya ya Uhehe baada ya
kushika utawala mnamo mwaka 1870.
Huyu aliwashinda kivita wababe wa Kinitole na kuyaunganisha makabila ya Iringa, watu
waliokuja kuitwa Wahehe na wakoloni
hapo baadaye kutokana na mlio wao wa kivita wanapotupa mikuki kwa kusema he he
he! wakiashiria hatari.
Kutoka Mutwa huyu ndipo alifuatia kutawala Mukwavinyika, mtoto wa pili wa Munyigumba,
ambaye jina lake mtawala huyu liliwashinda wakoloni kulitamka na hivyo
kufupisha kwa kutamka Mkwawa.
Mkwavinyika alianza kutawala akiwa na
miaka 19 na aliyapiga vita makabila
yote yaliyozunguka himaya yake na kuwashinda watu kama kina Chabuluma, Mtwa wa Wangoni na Merere,
shemeji wa Mtwa wa Wasangu. Mukwavinyika alipigana pia na wakoloni
wa Kijerumani.
Msomaji, simulizi hizi za Wahehe ni
ndefu sana na zenye mambo mengi mno, ikiwemo kujipa majina ya kujitapa
kulikofanywa kwa idhini ya Mutwa
baada ya kutenda matendo makuu, ushujaa wa kutupa mikuki, uwezo wa mbio za
kufukuza maadui, dawa za ushindi wa vita nakadhalika. Kwa sasa hapa panatosha
kumalizia simulizi hizi za Wahehe.
No comments:
Post a Comment