MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI

MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI
Tangazo la Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

KAUKI-Kidamali, Iringa

KAUKI-Kidamali, Iringa
Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Tuesday, January 7, 2014

HOTUBA YA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA TISA WA KAUKI JUNI 29 – 30, 2013, KIDAMALI – IRINGA


Ndugu Mgeni Rasmi,
Ndugu Wageni Waalikwa;
Wanaukoo na Jamii yote inayounda KAUKI;
Ndugu Majirani, Marafiki na Jamii yote Iliyojumuika Nasi;
Mabibi na Mabwana;

Kamwene…, Munogage…, Makasi…,

Awali ya yote, nimwombe Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, uzima na Baraka, awape nguvu, afya na amani, wote mliokusanyika katika Mkutano huu wa 9 wa KAUKI.

Pili, nimwombe Mwenyezi Mungu, awaepushe na hatari, rapsah na ubaya wowote ulioelekezwa kwenu; awalinde kutoka saa hii ya ufunguzi wa Mkutano hadi kesho wakati wa kuhitimisha shughuli hii muhimu kwa mwaka huu 2013.

Tatu, nawaomba wote tusimame kwa dakika moja (1) kuwakumbuka ndugu zetu ambao wametangulia mbele ya haki kutoka mwaka jana hadi mwezi Juni mwaka 2013. Ndugu waliotangulia mbele za haki ni:
  1. Luhanage Ponsiano Sigatambule Kivenule
  2. Flomina Pangalas Kivenule
  3. Gidagumhindi (Cecilia) Sigatambule Kivenule
  4. Atanas
  5. Mzee wetu Babu Hussein Tavimyenda Tagumtwa Kivenule

Mwenyezi Mungu azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi, Amina.

Baada ya utangulizi huo mfupi, ni furaha kubwa kujumuika na hadhara hii siku ya leo.  Ni matumaini yangu kuwa wote ni wazima wa afya na pia uwepo wenu unaonesha namna mnavyothamini shughuli hii muhimu itakayofanyika kwa muda wa siku mbili; yaani leo na kesho, hali kadhalika kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa 9 wa KAUKI unafakiwa.   

Ni furaha iliyoje kuwa nanyi katika hadhara hii. Ni matumaini yangu kuwa, wote ni wazima wa afya na kuwepo kwenu pia kuonesha jinsi mnavyothamini shughuli ambayo tutaifanya kwa siku mbili, yaani leo na kesho katika kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI unafanikiwa.

Ndugu Mgeni Rasmi;  nianze kutoa historia fupi ya umoja huu. KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka 2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi. Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ulianzishwa rasmi mnamo Desemba 17 - 18, 2005 Kijijini Kidamali. Harakati za kuanzishwa kwa KAUKI zilianza mwezi Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa kufanya mkutano wa kwanza wa mashauriano. Harakati nyingine na kuunda kamati za maandalizi zilielekezwa upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa upande wa Kidamali, Mkutano wa kwanza wa maandalizi ya Mkutano Mkuu ulifanyika mwezi Mei ambapo wajumbe toka Dar es Salaam walishiriki katika majadiliano, kuchagua viongozi wa kuunda kamati ya maandalizi na kuhamasisha.

Ndugu Mgeni Rasmi; Umoja wa Ukoo wa Kivenule ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006 katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali, Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, kulienda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule na kuwa Katiba Rasmi; hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo, kulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa Kanda, uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.

Ndugu Mgeni Rasmi; Huu ni Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI; na tayari mikutano mingine Nane imekwisha fanyika, mitatu kijijini Kidamali na mkutano moja kijijini Irole, Nduli Magubike, Igowole-Mufindi na Jijini Dar es Salaam. Huu ni mzunguko mwingine tena baada ya kumaliza kanda zote. Pengine mkutano huu utashauri namna nyingine ya uendeshaji wa mikutano ya namna hii.

Malengo ya KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; malengo makuu ya KAUKI ni kujaribu kwa kila hali kwa kutumia ujuzi na maarifa, kuinua uwezo wa kielimu, kiuchumi na kimaendeleo, kwa wanajamii wanaounda umoja huo, kwa kutumia rasilimali mbalimbali zinazopatika katika nchi ya Tanzania na hususani katika maeneo wanayoishi; ikiwa ni pamoja kuihamasisha jamii hii kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kupunguza umaskini unaowakabili.

KAUKI imeanzishwa kukidhi shida na mahitaji ya jamii iliyounda umoja huu na hususani katika maeneo lengwa ya elimu, afya, uchumi na maendeleo, kwa kushirikisha mawazo, fikra, ujuzi na maarifa ya kila mwanaukoo, katika mikutano mikuu na mikutano midogo midogo, ambayo inaandaliwa na wanaukoo wenyewe. Kwa kukutana pamoja, fikra za kujenga, ujuzi, uzoefu, kujengewa uwezo na maarifa, huunganishwa pamoja na kisha kupanga mikakati mbadala ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha.

Ndugu Mgeni Rasmi; malengo KAUKI ni mengi na baadhi yake ni:
·         kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda
·         Kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa kusaidia ndugu katika elimu, afya na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa na unaendelea kuchangiwa. 
·         kuwa na sanduku lake la posta, tovuti. Kwa sasa ina tovuti  inayopatika kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com na inaboreshwa kupitia www.tagumtwa.blogoak.com  na www.kauki-kauki.blogspot.com   
·         Kuwa na Akaunti katika Benki – tayari imefungua katika Benki ya NMB, Iringa Mjini
·         kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti
·         kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake
·         kubuni na kutekeleza miradi ambayo itawasadia wanajamii. Mpango wa Mradi wa Alizeti-Irole, ambao bado haujaanza kutekelezwa.
·         kuwa na kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja na miradi mbalimbali. Ipo katika mchakato.
·         Kuchapisha kitabu toleo la kwanza cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2009-2013. Kazi inaendelea na taarifa mbalimbali zinaendelea kukusanywa.

Mafanikio
Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imefanikiwa kufanya yafuatayo:
·         kuendelea kufanyika kwa mikutano mkuu. Mikutano Mikuu nane tayari imefanyika Kidamali mara tatu, Irole, Nduli, Magubike, Igowole-Mufindi na mara moja moja.
·         kupanua wigo wa ushiriki kutoka Irole, Nduli, Itagutwa, Mgongo na Mufindi; Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro na maeneo mengine.
·         Kuongezeka kwa ufahamu na uelewa wa watu kuhusu KAUKI na mada zinazofundishwa
·         Kufahamiana baina ya wana-KAUKI kumeongezeka mara dufu
·         Kuanzishwa kwa Mfuko wa KAUKI
·         Imeanzisha blogs ambazo zinabeba taarifa mbalimbali za KAUKI na wana-KAUKI kwa ujumla.

Changamoto
Ndugu Mgeni Rasmi; Changamoto zinazoikabili KAUKI ni pamoja na
·         Ushiriki duni wa wanaukoo katika mikutano mikuu.
·         Kasi ndogo na moyo wa kuchangia mfuko wa kusaidia wanaukoo
·         Kutokidhi gharama za kuandaa mikutano hii kwa sababu michango inakuwa ni kidogo
·         Kutofikia malengo ya mipango tunayojiwekea
·         Ndugu wa mijini kuwa na mwamko mdogo wa kuunga mkono jitihada hizi

Matarajio katika Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI
Ndugu Mgeni Rasmi; Kama Ratiba inavyoonesha, hayo ndiyo yatakayofanyika katika siku mbili za Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI. Lakini, tunategemea kuwa na Mada kadhaa ikiwemo ya Chimbuko Historia ya Ukoo ambapo tutaijadili kwa undani zaidi. Lakini pia, masuala mengine mfano elimu, maendeleo na ushirikiano wa dhati baina ya wanandugu yatapewa kipaumbele.

Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na kila ndugu/mwanaukoo atakuwa na kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake. Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.

Tutakuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi. Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu wa Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba na Nane wa KAUKI, maeneo yatakayotolewa uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo mbalimbali. Kwa kupeana elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo ni mbadala kwetu. Pia taarifa hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine kupata mwanga wa shughuli mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha maisha.

Matarajio ya Mbeleni
Ndugu Mgeni Rasmi; Mipango ya KAUKI kwa mwaka uliopita 2011 na 2012
·         Kuendeleza jitihada za kufungua ofisi Kidamali na kununua vifaa vya ndani ya ofisi kama vile kompyuta, printa na fenicha.
·         Kuchapisha kitabu cha historia ya wahehe ambapo ndani yake pia kutakuwa na taarifa za KAUKI.
·         Kuongeza wigo wa ushiriki katika mikutano; na
·         Kuhamasisha wana-KAUKI kuchangia mfuko

Hitimisho
Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imeendelea kujikita katika kuongeza uangavu na weledi kwa wanaukoo kutokana na kutambua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika dunia hii ya ushindani. Ugumu wa maisha, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, na changamoto mbalimbali ambazo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au kuathiriwa nayo. Tatizo la ufisadi wa raslimali za watanzania, rushwa katika huduma za jamii mfano kukosa dawa hospitalini, maji safi na salama, elimu duni na ukosefu wa ajira, vyote vinatuathiri sisi. KAUKI inaamini kuwa mwana-KAUKI mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kuamua hatma na mustakabali wa maisha yake ya sasa na baadaye. KAUKI haitarajii maisha bora kwa kila mwana-KAUKI au mtanzania mwingine yataletwa na wanasiasa au watu baki waliopo nje ya nchi yetu. Jukumu la maendeleo ni letu sisi wenyewe. Ndio maana tunahimiza watu kujitoa kwa hali na mali kuuchangia mfuko wetu ili uweze kuisaidia jamii yetu katika nyanja zote za kiuchumi, elimu, afya na maendeleo.

Ndugu Mgeni Rasmi, baada ya kusema hayo machache, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu ya Kidamali, Iringa, inakuomba Ufungue Rasmi Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI).

Karibu Sana


Imetolewa na:

Ndugu Donath Mhapa
Mwenyekiti wa KAUKI
Kwa Niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu  wa Tisa wa KAUKI

No comments:

Post a Comment