HOTUBA YA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU
WA 10 WA KAUKI, JUNI 28 – 29, 2014, KIDAMALI – IRINGA
Ndugu Mgeni Rasmi, Ndugu Wageni Waalikwa; Wanaukoo na Jamii
yote inayounda KAUKI;
Ndugu Majirani, Marafiki na Jamii yote Iliyojumuika Nasi; Mabibi
na Mabwana;
Kamwene…, Munogage…, Makasi…,
Awali
ya yote, nimwombe Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, uzima na Baraka, awape
nguvu, afya na amani, wote mliokusanyika katika Mkutano huu wa 10 wa KAUKI. Pili,
nimwombe Mwenyezi Mungu, awaepushe na hatari, rapsah na ubaya wowote ulioelekezwa
kwenu; awalinde kutoka saa hii ya ufunguzi wa Mkutano hadi kesho wakati wa
kuhitimisha shughuli hii muhimu kwa mwaka huu 2014.
Tatu,
nawaomba wote tusimame kwa dakika moja (1) kuwakumbuka ndugu zetu ambao
wametangulia mbele ya haki kutoka mwaka jana hadi mwezi Juni mwaka 2014. Ndugu
waliotangulia mbele za haki ni:
1.
Agnes Mapembe, Mtoto wa Marehemu
Sandra Kivenule, Mjukuu wa Kavilimembe Tavimyenda Kivenule
Mwenyezi
Mungu azilaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.
Baada
ya utangulizi huo mfupi, ni furaha kubwa kujumuika na hadhara hii siku ya
leo. Ni matumaini yangu kuwa wote ni
wazima wa afya na pia uwepo wenu unaonesha namna mnavyothamini shughuli hii
muhimu itakayofanyika kwa muda wa siku mbili; yaani leo na kesho, hali
kadhalika kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI unafakiwa.
Ni
furaha iliyoje kuwa nanyi katika hadhara hii. Ni matumaini yangu kuwa, wote ni
wazima wa afya na kuwepo kwenu pia kuonesha jinsi mnavyothamini shughuli ambayo
tutaifanya kwa siku mbili, yaani leo na kesho katika kuhakikisha kuwa Mkutano
Mkuu wa Kumi wa KAUKI unafanikiwa.
Ndugu
Mgeni Rasmi; nianze kutoa historia fupi
ya umoja huu. KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka
2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii
inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia
kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la
umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi. Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ulianzishwa
rasmi mnamo Desemba 17 - 18, 2005 Kijijini Kidamali. Harakati za kuanzishwa kwa
KAUKI zilianza mwezi Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa kufanya mkutano
wa kwanza wa mashauriano. Harakati nyingine na kuunda kamati za maandalizi
zilielekezwa upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa upande wa Kidamali,
Mkutano wa kwanza wa maandalizi ya Mkutano Mkuu ulifanyika mwezi Mei ambapo
wajumbe toka Dar es Salaam walishiriki katika majadiliano, kuchagua viongozi wa
kuunda kamati ya maandalizi na kuhamasisha.
Ndugu
Mgeni Rasmi; Umoja wa Ukoo wa Kivenule ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika
Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006
katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali, Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo
wa Kivenule, kulienda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na
Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule na kuwa Katiba Rasmi;
hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali
ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa
Ukoo, kulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa Kanda, uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na
hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.
Ndugu
Mgeni Rasmi; Huu ni Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI; na tayari mikutano mingine Nane
imekwisha fanyika, mitatu kijijini Kidamali na mkutano moja kijijini Irole, Nduli,
Igowole-Mufindi na Jijini Dar es Salaam na Mikutano 2 Magubike,. Huu ni
mzunguko mwingine tena baada ya kumaliza kanda zote. Pengine mkutano huu
utashauri namna nyingine ya uendeshaji wa mikutano ya namna hii.
Malengo ya KAUKI
Ndugu
Mgeni Rasmi; malengo makuu ya KAUKI ni kujaribu kwa kila hali kwa kutumia ujuzi
na maarifa, kuinua uwezo wa kielimu, kiuchumi na kimaendeleo, kwa wanajamii
wanaounda umoja huo, kwa kutumia rasilimali mbalimbali zinazopatika katika nchi
ya Tanzania na hususani katika maeneo wanayoishi; ikiwa ni pamoja kuihamasisha
jamii hii kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kupunguza umaskini
unaowakabili.
KAUKI
imeanzishwa kukidhi shida na mahitaji ya jamii iliyounda umoja huu na hususani
katika maeneo lengwa ya elimu, afya, uchumi na maendeleo, kwa kushirikisha
mawazo, fikra, ujuzi na maarifa ya kila mwanaukoo, katika mikutano mikuu na
mikutano midogo midogo, ambayo inaandaliwa na wanaukoo wenyewe. Kwa kukutana
pamoja, fikra za kujenga, ujuzi, uzoefu, kujengewa uwezo na maarifa,
huunganishwa pamoja na kisha kupanga mikakati mbadala ya kuweza kukabiliana na
changamoto zinazojitokeza katika maisha.
Ndugu
Mgeni Rasmi; malengo KAUKI ni mengi na baadhi yake ni:
·
kuwa na ofisi yake Kijijini
Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda
·
Kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa
kusaidia ndugu katika elimu, afya na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa
na unaendelea kuchangiwa.
·
kuwa na sanduku lake la posta,
tovuti. Kwa sasa ina tovuti inayopatika
kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com
na inaboreshwa kupitia www.tagumtwa.blogoak.com
na www.kauki-kauki.blogspot.com
·
Kuwa na Akaunti katika Benki –
tayari imefungua katika Benki ya NMB, Iringa Mjini
·
kuwa na vitendea kazi mfano
Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti
·
kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa
wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake
·
kubuni na kutekeleza miradi ambayo
itawasadia wanajamii. Mpango wa Mradi wa Alizeti-Irole, ambao bado haujaanza
kutekelezwa.
·
kuwa na kitengo cha Utaalam wa
Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja
na miradi mbalimbali. Ipo katika mchakato.
·
Kuchapisha kitabu toleo la kwanza
cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2009-2013. Kazi inaendelea
na taarifa mbalimbali zinaendelea kukusanywa.
Mafanikio
Ndugu
Mgeni Rasmi; KAUKI imefanikiwa kufanya yafuatayo:
·
kuendelea kufanyika kwa mikutano mkuu.
Mikutano Mikuu Tisa tayari imefanyika Kidamali mara tatu, Magubike mara tatu, Irole,
Nduli, Igowole-Mufindi na mara moja moja.
·
kupanua wigo wa ushiriki kutoka
Irole, Nduli, Itagutwa, Mgongo na Mufindi; Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro
na maeneo mengine.
·
Kuongezeka kwa ufahamu na uelewa wa
watu kuhusu KAUKI na mada zinazofundishwa
·
Kufahamiana baina ya wana-KAUKI
kumeongezeka mara dufu
·
Kuanzishwa kwa Mfuko wa KAUKI
·
Imeanzisha blogs ambazo zinabeba
taarifa mbalimbali za KAUKI na wana-KAUKI kwa ujumla.
Changamoto
Ndugu
Mgeni Rasmi; Changamoto zinazoikabili KAUKI ni pamoja na
·
Ushiriki duni wa wanaukoo katika
mikutano mikuu.
·
Kasi ndogo na moyo wa kuchangia
mfuko wa kusaidia wanaukoo
·
Kutokidhi gharama za kuandaa mikutano
hii kwa sababu michango inakuwa ni kidogo
·
Kutofikia malengo ya mipango
tunayojiwekea
·
Ndugu wa mijini kuwa na mwamko
mdogo wa kuunga mkono jitihada hizi
Matarajio katika Mkutano Mkuu wa 10
wa KAUKI
Ndugu
Mgeni Rasmi; Kama Ratiba inavyoonesha, hayo ndiyo yatakayofanyika katika siku
mbili za Mkutano Mkuu wa Kumi wa KAUKI. Lakini, tunategemea kuwa na Mada kadhaa
ikiwemo ya Chimbuko Historia ya Ukoo ambapo tutaijadili kwa undani zaidi.
Lakini pia, masuala mengine mfano elimu, maendeleo na ushirikiano wa dhati
baina ya wanandugu yatapewa kipaumbele.
Utambulisho
baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na kila ndugu/mwanaukoo atakuwa na
kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake. Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa
wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa utafutaji wa maisha bora. Mbinu za
kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali
za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.
Tutakuwa
na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka katika
maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi. Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu
wa Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba, Nane na Tisa wa KAUKI, maeneo yatakayotolewa
uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo mbalimbali. Kwa kupeana
elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri
na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo ni mbadala kwetu. Pia taarifa
hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine kupata mwanga wa shughuli
mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha maisha.
Matarajio ya Mbeleni
Ndugu
Mgeni Rasmi; Mipango ya KAUKI kwa mwaka uliopita 2014 na 2015
·
Kuendeleza jitihada za kufungua
ofisi Kidamali na kununua vifaa vya ndani ya ofisi kama vile kompyuta, printa
na fenicha.
·
Kutafuta hati ya Kimila ya Eneo la
Kihistoria la Mlafu
·
KAUKI kufuatilia kwa karibu suala
la Elimu kwa Watoto katika Kanda
·
Kuchapisha kitabu cha historia ya
wahehe ambapo ndani yake pia kutakuwa na taarifa za KAUKI.
·
Kuongeza wigo wa ushiriki katika
mikutano; Kuhamasisha wana-KAUKI kuchangia mfuko
Hitimisho
Ndugu
Mgeni Rasmi; KAUKI imeendelea kujikita katika kuongeza uangavu na weledi kwa
wanaukoo kutokana na kutambua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika dunia
hii ya ushindani. Ugumu wa maisha, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, na
changamoto mbalimbali ambazo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au
kuathiriwa nayo. Tatizo la ufisadi wa raslimali za watanzania, rushwa katika
huduma za jamii mfano kukosa dawa hospitalini, maji safi na salama, elimu duni na
ukosefu wa ajira, vyote vinatuathiri sisi. KAUKI inaamini kuwa mwana-KAUKI mwenyewe
ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kuamua hatma na mustakabali wa maisha yake ya
sasa na baadaye. KAUKI haitarajii maisha bora kwa kila mwana-KAUKI au mtanzania
mwingine yataletwa na wanasiasa au watu baki waliopo nje ya nchi yetu. Jukumu
la maendeleo ni letu sisi wenyewe. Ndio maana tunahimiza watu kujitoa kwa hali
na mali kuuchangia mfuko wetu ili uweze kuisaidia jamii yetu katika nyanja zote
za kiuchumi, elimu, afya na maendeleo.
Ndugu
Mgeni Rasmi, baada ya kusema hayo machache, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi
ya Mkutano Mkuu ya Kidamali, Iringa, inakuomba Ufungue Rasmi Mkutano Mkuu wa 10
wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI).
Karibu
Sana
Imetolewa
na:
Ndugu
Faustino Kivenule
Mwenyekiti wa KAUKI
Kwa Niaba ya Kamati ya Maandalizi
ya Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI
No comments:
Post a Comment